Tunawezaje Kuishi na Virusi vya Corona (Cov)?Tujifunze Tulikotoka.
Tunawezaje Kuishi na Virusi vya Corona (Cov)?Tujifunze Tulikotoka.

Baada ya shirika la umoja wa kimataifa linalojishughulisha na masuala ya afya (WHO) kutamka kwamba kuna uwezekano mkubwa wa Virusi vya Corona kutoondoka kama virusi vingine vya HIV na surua; watu wengi wamekuwa wakijiuliza maisha mapya na kirusi hiki hatari yatakuwaje.
Ni ukweli usiopingika kuwa uwepo wa virusi vya Corona unaongeza mzigo wa magonjwa kwa nchi zote zinazoendelea na zilizoendelea. Wakati nchi zilizoendelea zikiwa kwa kiasi kikubwa wameweza kupambana na magonjwa ya maambukizi, kwa nchi zinazoendelea ambako magonjwa ya kuambukizwa kama HIV, Ebola, kipindupindu, malaria bado ni tishio na yanatumia rasimali kubwa katika kupambana nayo, virusi vya corona ni mzigo mwingine mzito kwa nchi hizi.
Lakini pamoja na hisia hizo, nchi hizi kutokana na uzoefu mkubwa wa kuweza kupambana na magonjwa ya kuambukiza, uzoefu huu unaweza kutumika katika kuweza kuishi na kirusi hiki bila madhara makubwa.
Kwa nchi kama Tanzania ambako tangia tulivyopata kisa cha kwanza cha mgonjwa wa corona hapo mnamo mwezi Machi tumekuwa tunaishi na kirusi (kwa maana kwamba shughuli za uchumi ziliendelea kama kawaida kwa kuchukua tahadhari) tunaweza kuwa mfano mzuri wa jinsi ya kuishi na kirusi hiki.
Tumeshuhudia jinsi mifumo ya afya ambayo iliwekwa kupambana na magonjwa mengine ya kuambukizwa hasa virusi vya ukimwi inavyotumika sasa haswa katika utoaji wa elimu na tahadhari kwa jamii ambayo haiwezi kufikika haraka. Mifumo hii ni pamoja na kuwatumia wafanyakazi wa afya wa jamii (Community health worker) kutoa elimu kwa maeneo ya vijijini na mijini.

Lakini hebu tuangazie nyuma ni jinsi gan tulivyoweza kuishi na kirusi cha HIV ambacho wakati wa kugundulika kwake kilizua sana taharuki kwa wakati huo, taharuki ambayo wengi waliokuwepo wakati huo wameweza kuifananisha na taharuki ya sasa. Ingawa uzoefu na mafunzo jinsi ya kuishi na HIV inaweza ikawa haitoshi kwa kukabiliana na virusi vya Corona kwa sababu ya tofauti zake katika uambukizaji ila zinaweza weka msingi wa kuanzia katika kujua jinsi ya kuishi na virusi vya corona.
Mambo makuu matatu yalifanyika katika kupambana na virusi vya Ukimwi haswa siku za mwanzo:
- Elimu kupitia njia mbalimbali kuanzia vyombo vya habari, sanaa, maeneo ya kuabudu, sehemu za kazi, katika vyombo vya usafiri. Kila mmoja alijua Ukimwi unaua na unauweza kuepuka kwa kuacha ngono (abstinence) kuwa mwaminifu (Be faithful to one partner) Tumia condom (Use Condom).
- Ugawaji wa kondomu za bure kwa makundi hatarishi.
- Kampeni za kuhamasisha kupima na kutowanyanyapaa waathirika.
Na kwa siku za karibuni,
- Kampeni za kujikubali na kujitokeza kwa hiari kupima na kutumia dawa.
Kwa nchi kama Tanzania, suala la elimu ya Virusi vya Corona kupitia njia mbalimbali zilizotumika kipindi cha HIV zimetumika kwa kiasi kikubwa na matangazo yapo kila mahali yakitoa elimu kuhusu virusi hivi na namna ya kujikinga na nini cha kufanya uonapo dalili zinaashiria kuambukizwa na kirusi hiki. Na kwa sasa kutokana na ongezeko la teknolojia kumekuwa na matangazo haya hata mtu anapopiga simu, kabla ya simu kuunganisha mitandao yote ya simu imeweka sauti maalumu kutoa tahadhari ya Virusi hivi. Ingawa katika njia hii, njia ya sanaa ambayo ilionyesha sana mafanikio katika utoaji wa elimu wa maambukizi ya virusi ya ukimwi imesahaulika kwa kiasi fulani. Hii inaweza kuchangiwa na mambo mengi ikiwemo labda ukosefu wa bajeti kuhamasisha wasanii au wasaniii kutokuwa na utayari wa kutumia sanaa zao kuwa wahamasishaji. Sina hakika. Ila ni muhimu Baraza la sanaa la taifa kuona jinsi gani inaweza kutumia sanaa katika utoaji wa elimu dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Katika kujiepusha kabisa na virusi vya corona inahamasishwa kukaa nyumbani na kuepuka safari zisizo za lazima, ikibidi kutoka vaa barakoa na hakikisha unanawa mikono yako. Hii inafanana sana na HIV ambapo katika kuepuka HIV ilishauriwa kuacha kufanya mapenzi au kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu na ukishindwa tumia kondomu. Ila kutokana na waathirika zaidi walikuwa ni watu kutoka mazingira maskini ilikuwa inawawia vigumu kumudu gharama za kondomu ambazo ilikuwa ni kama shillingi 100 hadi 500 ya kitanzania. Hii inaonekaana hata sasa kwenye hamasa ya kunawa mikono na kuvaa barakoa. Nchini Tanzania ni asilimia 60 % tu ya kaya wanauwezo wa kupata maji masafi ya kunawa na sabuni (Unicef,2016). Kwa kutambua ili serikali iliweza kuhamasisha maeneo yote ya mkusanyiko kuwa na maji na sabuni na kutotoa huduma kwa watu wasiosafisha mikono. Hili linapaswa kuendeleza na serikali inaweza kutoa muongozo na ikawa ni sehemu ya sheria kwamba wahusika wote wa maeneo ya mkusanyiko kuhakikisha wakati wote maeneo hayo yana maji na sabuni na ni lazima kabla ya kupata huduma mtu yeyote anawe mikono.

Kwa upande wa barakoa ambazo nyingi zinapatikana kwa wastani wa shilling 1000 hadi 5000 kwa moja, ambapo kwa mtu ambaye anatoka kila siku inabidi awe na angalau barakoa si chini ya moja, hii inaweza ikawa changamoto kwa watu takaribani milioni 14 ambao wanaishi katika umaskini uliopitiliza. Kwa kutumia mifumo kama ya TASAF ya kutambua kaya maskini, au mfumo wa ugawaji chandarua zenye dawa ya kuua mbu wa malaria kwa kaya maskini Serikali na wadau wengine wanaweza kuja na mfumo wa ugawaji barakoa kwa kaya maskini kwa kila baada ya muda wa miezi sita.

Ni dhahiri kwamba mafanikio ya kupigana na Corona yatatokana na mabadiliko katika tabia ambapo mabadiliko haya ni pamoja na kila mmoja kutambua Corona ipo, inaepukika na sio ugonjwa wa kuficha. Katika kufanikisha hili kama ilivyokuwa kampeni za kuhamasisha upimaji wa virusi wa UKIMWI kwa watu kujitokeza hadharani ili kukabiliana na unyapaa ni dhahiri juhudi zinatakiwa kufanyika kuhamasisha watu wenye dalili kujitokeza hadharani na kutoa elimu haswa juu ya njia walizotumia katika kukabiliana na corona. Hiii ni pamoja na kuwepo na takwimu sahihi juu ya kesi mpya na vifo kwa mkoa ikibidi hadi kwa ngazi ya kijiji. Hiii itawawezesha wadau mbalimbali kujua wapi wanaweza kuiongezea nguvu serikali katika kupambana na maambukizi haya.
Usalama Makazini Sekta Rasmi
Corona inatoa changamoto ya upitiaji upya wa sera na sheria za usalama wa kazini, haswa katika kukabiliana na magonjwa ambukizi.
Usalama Makazini Sekta isiyo rasmii
Kutumia vyama vilivyopo katika sehemu mbalimbali za sekta isiyo rasmi. Uzuri kwa Tanzania mifumo ya vyama vidogo vidogo vya kusaidiana katika raha na shida imekuwa ni moja ya mifumo inayoheshimika sana haswa katika sekta isiyo rasmi. Hii ni kuanzia vyama vya makonda na madereva, vyama vya wauzaji sokoni, vyama vya wafanya usafi, vyama vya kijamii, nk. Serikali na wadau wengine wanaweza kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na vyama hivi ili kuweza kuhakikisha kupitia miongozo ya usalama kazini iliyotolewa na serikali inafuatwa kwa usahihi na uaminifu miongoni mwa wanachama wake.
Kitendawilii kigumu ni jinsi gani tunavyoweza kuhakikisha usalama kwa wanafunzi haswa wale wa elimu ya msingi, hii ni kutokana na mifumo iliyopo kwa sasa haitoshi kuhakikisha usalama kwa watoto hawa. Hii ikiwemo mifumo ya maji na usafi mashuleni kuwa ni changamoto. Na hiki ni kitendawili ambacho bado hata katika mapambano dhidi ya VVU hatujaweza kukitegua.
Kwa Pamoja tunaweza kutokomeza virusi vya Corona Tanzania.
Ahsante sana kwa ujumbe huu. Umeelezea vizuri sana. Pamoja, tunaweza kutokomeza Corona Tanzania.